Ruka hadi kwenye maudhui

Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI | ITOLEWE MARA MOJA

Frontier Minerals yakaribisha kuchaguliwa kwake kwa mradi wa Mrima Hill

NAIROBI, 19 Novemba 2026 – Frontier Minerals inakaribisha tangazo la Serikali ya Kenya linalothibitisha kuchaguliwa kwake kwa Mradi wa Uendelezaji wa Niobium, Madini Adimu (rare earths) na Madini Mengine wa Mrima Hill (Mrima Hill Niobium, Rare Earth Elements and Other Minerals Development Project) katika Kaunti ya Kwale.

Pendekezo la Frontier linalenga kujenga uwezo wa kusindika na kusafisha madini nchini Kenya, fursa kwa wasambazaji wa Kenya, ajira na mafunzo ya kiufundi, pamoja na kusaidia jamii na maendeleo yake. Hatua inayofuata itakuwa kuweka msingi wa kiufundi, wa kibiashara na wa kiudhibiti utakaowezesha mradi kuendelea kwa njia bora zaidi.

Brad Barnett, Mwanachama Msimamizi (Managing Member) wa Frontier Minerals, alisema:

"Ni heshima kubwa kwetu kuchaguliwa na Serikali ya Kenya, na tunatambua jukumu linaloambatana na kuendeleza rasilimali yenye umuhimu mkubwa kiasi hiki kwa Wakenya na kwa dunia nzima.

"Tutafuata njia iliyofanyiwa utafiti wa kina na yenye heshima ili kupata thamani bora zaidi kutoka kwa miamba hii yenye madini muhimu, tukilenga kuhakikisha Kenya inanufaika na mnyororo wa thamani, ikiwemo kusindika na kusafisha madini ndani ya nchi. Tunakusudia kuleta fursa za kudumu kwa wafanyakazi wa Kenya, biashara na uchumi kwa jumla kupitia kujenga uwezo na uwekezaji unaolenga mahitaji mahususi, huku tukitoa kipaumbele kwa usimamizi wa mazingira na utendaji bora wa kimazingira.

"Hatua inayofuata italenga kubainisha njia zinazofaa zaidi na zinazojali mazingira za uchimbaji, usindikaji, usafishaji na maendeleo ya jamii. Tumejitolea kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika na jamii za wenyeji ili kuhakikisha mradi unaendelea kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kenya, na kwa kufuata mbinu bora za sekta."

Utaalamu wa kiufundi na usindikaji nchini Kenya

Muungano wa Frontier Minerals unajumuisha Bunker Hill Mining Corp., American Resources Corporation na ReElement Technologies Corporation. Unaleta pamoja utaalamu unaokamilishana wa uendelezaji wa rasilimali za madini, minyororo ya ugavi wa nyenzo muhimu na teknolojia za hali ya juu za usafishaji.

Bunker Hill Mining Corp. (TSX: BNKR; OTCQB: BHLL) inaleta uzoefu wa uchimbaji na usindikaji wa madini. Ina mali (assets) nne za madini muhimu nchini Marekani, na timu ya uongozi ambayo imefanya kazi kwa mapana barani Afrika. Mgodi wa Bunker Hill ulioko Idaho, uliofungwa mwaka 1981, ulizalisha madini yaliyokolezwa (concentrate) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 45 mnamo 29 Juni 2026. Teck Resources ilitangaza mnamo Machi 2025 kwamba inawekeza katika kampuni hiyo ili kujihakikishia madini yaliyokolezwa ya zinki na madini ya risasi (lead) kwa ajili ya kiwanda chake cha kuyeyusha madini cha Trail nchini Kanada. Usafirishaji kwenda Trail ulianza Julai 2026, na sasa usafirishaji na mauzo ya mara kwa mara ya madini yaliyokolezwa yanaendelea. Kufunguliwa upya kwa mgodi kunategemea makubaliano ya mwaka 2018 kati ya kampuni na Shirika la Kulinda Mazingira la Marekani (US Environmental Protection Agency) pamoja na Idara ya Haki (Department of Justice). Chini ya makubaliano hayo, Bunker Hill ilisuluhisha dhima yake kuhusu uchafuzi wa kihistoria wa eneo hilo kwa kukubali kulipa dola za Marekani milioni 20 (US$20 million) za gharama za awali za kutibu maji ambazo mmiliki wa zamani wa mgodi hakuzilipa, na kulipia gharama za kutibu maji ya mgodi kuanzia hapo na kuendelea. Marekebisho ya Desemba 2021 yalipanga upya dola za Marekani milioni 17 (US$17 million) za malipo hayo ili zilipwe katika miaka ya uzalishaji wa mgodi. Mgodi huo sasa unazalisha.

American Resources inaendesha jukwaa la shughuli mbalimbali za nyenzo muhimu kupitia mkakati wake wa Platform Orchestration. Inaratibu upatikanaji wa rasilimali, ukusanyaji wa malighafi, usindikaji wa viwandani na ubia wa kimkakati, ili kuwezesha kunufaika zaidi na mnyororo wa thamani.

ReElement ni kampuni yenye makao yake Marekani ya ugeuzaji wa nyenzo za hali ya juu. Inaendesha mfumo wa utenganishaji na utakasaji, unaotumia teknolojia yake yenyewe yenye hataza inayotegemea kromatografia (chromatography), kugeuza malighafi mbalimbali za madini kuwa nyenzo muhimu zenye usafi wa kiwango cha juu na zinazokidhi vipimo maalum vinavyotakiwa. Mchakato wake wa usafishaji, unaotumia vitengo vinavyounganishwa (modular) na unaojali mazingira, umeundwa kupunguza matumizi ya kemikali na athari kwa mazingira. Pia unawezesha uwezo wa hali ya juu wa usafishaji kuwekwa karibu na rasilimali za madini kwa ufanisi, jambo linalosaidia usindikaji ndani ya nchi, kunufaika zaidi na mnyororo wa thamani, na minyororo ya ugavi wa madini muhimu inayoweza kupanuliwa kibiashara.

ReElement Technologies imethibitisha ufanisi wa kiufundi wa teknolojia yake ya utenganishaji na utakasaji kwa madini 15 adimu (rare earths) na muhimu, na inazalisha kibiashara bidhaa kadhaa za nyenzo muhimu zenye usafi wa kiwango cha juu na zinazokidhi vipimo maalum vinavyotakiwa, kwa ajili ya wateja. Kampuni inapanua kiwanda chake cha usafishaji wa madini adimu (rare earths) na madini muhimu kilichoko Marion, Indiana, nchini Marekani. Kiwanda hiki, kinachoshughulikia elementi nyingi na malighafi za aina nyingi, kingekuwa mfano wa kurejelewa katika kuweka uwezo wowote wa hali ya juu wa usafishaji nchini Kenya, kwa kutegemea leseni, idhini zinazohitajika, ili kusaidia usindikaji na usafishaji wa humu nchini badala ya kusafirisha nje ya nchi madini yaliyokolezwa. Usafishaji ndani ya nchi unatarajiwa kufanya thamani kwa Kenya ya madini yatakayozalishwa Mrima Hill iwe juu zaidi kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo lingeleta fursa kubwa za kiuchumi kwa jamii za wenyeji, Serikali na uchumi wa Kenya kwa jumla.

Mrima Hill ina miamba yenye niobium pamoja na madini adimu (rare earths). Kutathmini uwezekano wa kutekeleza mradi na kubainisha njia bora ya kuuendeleza na kuuendesha kunahitaji uelewa wa kina wa jinsi madini haya yanavyoweza kuchimbwa, kusindikwa, kusafishwa na kuuzwa, huku ushiriki wa Wakenya na usimamizi wa mazingira vikizingatiwa kwa makini katika kipindi chote cha uendelezaji wa mradi.

Utafiti kamili wa uwezekano wa kutekeleza mradi (feasibility study) ungefanywa, baada ya Leseni ya Utafutaji Madini na idhini zinazohitajika kutolewa, ili kubainisha njia inayofaa zaidi ya kutekeleza shughuli hizi, kwa kuzingatia masuala ya kijamii, kiufundi, kimazingira, kibiashara na kisheria. Utafiti huu ungeainisha na kusanifu mgodi na kiwanda cha usindikaji ambavyo vingejengwa, kwa kutegemea leseni, idhini zinazohitajika, na ndio utafiti huru ambao ombi la Leseni ya Uchimbaji Madini na ufadhili vingeutegemea. Ungehusu:

  • Utoboaji wa mashimo ya kubaini rasilimali, kwa viwango vya kimataifa vya utoaji ripoti.
  • Majaribio ya metalajia na usindikaji wa kiwango cha mtambo wa majaribio (pilot).
  • Upangaji wa mgodi, miundomsingi, umeme na maji.
  • Tathmini za mazingira, za kijamii na za mila na kitamaduni.
  • Gharama, masoko na uchambuzi wa kiuchumi wa mradi.

Ushiriki wa Wakenya na ushirikishwaji wa jamii

Frontier inatambua umuhimu wa kimazingira, kitamaduni na kijamii wa Mrima Hill, na umuhimu wa kuhakikisha jamii za wenyeji zinashirikishwa kwa njia yenye maana kadri mradi unavyoendelea. Muungano umejitolea kushauriana kwa uwazi na jamii za wenyeji na mamlaka husika.

Hatua za kulinda mazingira na jamii pia zitakuwa kiini cha uendelezaji wa mradi. Muungano utafanya tathmini zinazohitajika ili kubaini athari zinazoweza kutokea, kuweka hatua zinazofaa za kuzipunguza, na kuhakikisha mradi unasanifiwa kwa mujibu wa sheria na masharti ya udhibiti ya Kenya.

Mbinu inayopendekezwa na muungano inajumuisha kujenga uwezo wa watu, wa kiufundi, wa kitaaluma na wa kibiashara, ili kuleta fursa kwa raia na biashara za Kenya kushiriki katika uendelezaji na utekelezaji wa mradi.

Hatua zinazofuata

Kuchaguliwa kwa muungano ni hatua muhimu katika uendelezaji wa Mrima Hill na ni mwanzo wa awamu inayofuata ya kazi. Frontier inatarajia kushirikiana na mamlaka husika za Kenya ili kuendeleza utafiti kamili unaohitajika wa uwezekano wa kutekeleza mradi (feasibility study), tathmini za mazingira na za kijamii, pamoja na shughuli za ushirikishwaji wa jamii.

Mradi utaendelea kwa mujibu wa mfumo wa udhibiti wa Kenya. Shughuli zozote za baadaye za utafutaji, uendelezaji na utekelezaji wa uchimbaji, usindikaji, usafishaji na usimamizi wa mazingira zitategemea kutolewa kwa leseni na vibali vyote vinavyohitajika.

Kuchaguliwa si leseni ya kuchimba madini. Muungano uko tayari kuanza mchakato wa leseni, kwa kufuata sheria za Kenya na mwongozo wa mamlaka husika. Mchakato huo unajumuisha:

  • Ombi la Leseni ya Utafutaji Madini kwa Ministry of Mining, Blue Economy and Maritime Affairs.
  • Ushirikishwaji wa jamii na idhini zinazotakiwa chini ya Sheria ya Madini (Mining Act).
  • Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii na leseni kutoka NEMA.
  • Utafutaji madini na utafiti kamili wa uwezekano wa kutekeleza mradi (feasibility study), ambavyo vinaweza kuanza tu baada ya Leseni ya Utafutaji Madini (ambayo bado haijatolewa) na idhini zinazohitajika kutolewa.
  • Ombi la Leseni ya Uchimbaji Madini, likijumuisha Mkataba wa Maendeleo ya Jamii.

– MWISHO –

Kuhusu Frontier Minerals

Frontier Minerals ni muungano wa kampuni za uendelezaji wa madini muhimu unaojumuisha Bunker Hill Mining Corp. (TSX: BNKR; OTCQB: BHLL), American Resources Corporation (NASDAQ: AREC) na ReElement Technologies Corporation. Muungano unaleta pamoja utaalamu unaokamilishana wa uendelezaji wa rasilimali za madini, minyororo ya ugavi wa nyenzo muhimu, na teknolojia za hali ya juu za usindikaji na usafishaji, ili kusaidia uendelezaji wa kuwajibika wa rasilimali za madini za kimkakati nchini Kenya. Frontier Minerals inalenga kuendeleza mkakati kamili wa uendelezaji, kuanzia mgodini hadi nyenzo zilizosafishwa, unaosisitiza usindikaji na usafishaji ndani ya nchi, ushiriki wa wenyeji katika uchumi, utunzaji wa mazingira na kunufaika kwa muda mrefu na mnyororo wa thamani. Kupitia uwezo wa pamoja wa wanachama wake, Frontier inanuia kusaidia ujenzi wa minyororo ya ugavi wa madini muhimu inayoweza kudumu kibiashara na inayoimarisha nafasi ya Kenya katika masoko ya kimataifa ya nyenzo za hali ya juu.

Maswali ya vyombo vya habari: media@frontier.ke

Pakua PDF